UGONJWA WA MDONDO/KIDERI (NEWCASTLE)
Mdondo/Kideri (Newcastle Disease)Maelezo
Ni ugonjwa unaosababishwa na virusi ambao hushambulia aina zote za spishi za ndege, ijapokuwa kuku ndio aina
inayoathirika zaidi. Binadamu na wanyama wengine pia wanaweza kuambukizwa. Ugonjwa huathiri mifumo ya
fahamu, njia ya chakula na hewa.
Jinsi Ugonjwa Unavyoenea
• Chanzo cha maambukizi ni maji, chakula kilichochafuliwa na kinyesi cha kuku wagonjwa. Pia maambukuzi
huweza kupitia mfumo wa hewa kutoka kwa kuku wagonjwa.
• Kuku, vifaa vya kazi na bidhaa zitokanazo na kuku (nyama, mayai, manyoya na mbolea) kutoka mashamba
yenye ugonjwa zinaweza kueneza ugonjwa kutoka shamba moja hadi jingine.
• Vifaranga wanaweza kupata maambukizi kutoka vituo vya kutotolea vifaranga kutokana na maganda ya
mayai yaliyochafuliwa.
Dalili
• Vifo vya ghafla vya idadi kubwa ya kuku katika shamba/banda
• Kuku wanatetemeka na kushindwa kutembea
• Kuku hupooza miguu, mabawa na kupinda shingo; na hujizungusha mahali alipo
• Kuku huharisha kinyesi cha kijani na wakati mwingine chenye mchanganyiko wa rangi ya njano
• Kuku huzubaa na kuacha kula
• Kuku hukohoa, hupiga chafya na kupumua kwa shida
• Vifo vinaweza kufikia asilimia 100, kutegemea na umri na aina ya ndege
Uchunguzi wa Mzoga(POST MORTEM LESIONS)
Ugonjwa huathiri zaidi mfumo wa hewa na njia ya chakula, hivyo mabadiliko yanayoonekana kwenye mzoga ni
pamoja na:
• Madoa ya damu kwenye mfumo wa hewa
• Kamasi nzito zenye rangi ya njano kwenye koromeo
• Utandu mweupe kwenye mifuko ya hewa
• Bandama kuvimba
• Uvimbe kwenye kichwa na eneo la shingo
• Madoa madogo madogo ya damu kwenye kifua, mafuta na utandu wa tumboni
• Damu kuvia kwenye mfumo wa usagaji chakula - juju, firigisi, tumbo na utumbo
Tiba
• Hakuna tiba ya ugonjwa huu ila kuku wapewe antibiotiki.
• Pata ushauri wa daktari.
Kuzuia na Kinga
• Weka utaratibu wa kuhakikisha wafanyakazi , wageni na ndege hawaingii hovyo kwenye shamba/banda
• Angamiza mizoga yote kwa njia stahiki kwa kuchoma moto au kufukia kwenye shimo refu ardhini.
• Hakikisha banda la kuku lina hewa ya kutosha na epuka msongamano mkubwa wa kuku.
• Fanya usafi wa mara kwa mara kwenye vyombo vya kuwekea maji na chakula, pamoja na mabanda ya
kuku.
• Zuia uingizaji holela wa kuku wageni wasiochanjwa kwenye shamba/banda. Kuku wanaoingia shambani/
bandani watoke maeneo yasiyokuwa na ugonjwa.
• Tenganisha kuku kufuatana na umri
• Maeneo yenye ugonjwa yawekwe chini ya karantini na mabanda yapulizwe dawa
• Kuku wapewe Chanjo tangu vifaranga wa umri wa siku 3, baada ya wiki 3 – 4, na baadaye kila baada ya
miezi 3.